E FM

E FM
SIKILIZA 93.7 E FM KILA SIKU

Tuesday, June 17, 2014

MIAKA MITATU YA MATESO...KUCHOMWA NA PASI, KUNG'ATWA..BINTI AELEZA KISA KIZIMA

“Nilipofika tuliishi vizuri, lakini 2012 alibadilika na kuanza kuniadhibu, mara alinituhumu kutokufagia au kutopiga deki vizuri au chakula kuwa na chumvi nyingi.
Mwanzoni alitumia fimbo alipohisi siumii alianza kuning’ata na kunichoma na pasi,” alisema.
“Alinikataza kulia kwa sauti na kunitisha kuwa ataniua au kuniroga nikimwambia mtu yeyote yale aliyokuwa ananifanyia.”
Yusta anasema kuwa tajiri yake huyo alibadilika zaidi baada ya kuondoka kwa mumewe ambaye hajui kama waliachana au alihama kikazi.
“Mwaka 2012 mumewe aliondoka na hapo ndipo matatizo yalizidi kwani hata mwanaye ambaye yuko kidato cha tatu alimpeleka shule ya bweni hivyo tulibaki wawili tu na hakukuwa na mtu wa kunisaidia,” anasema.
“Alinining’ata kila sehemu katika mwili wangu na alipoona damu imejaa mdomoni alitema na kisha kuendelea kuning’ata mpaka pale aliporidhika. Wakati mwingine alining’ata hadi usoni.”
Alisema alimfungia geti na kuondoka na funguo kila alipotoka kwenda kazini na alipomtuma sokoni alimuamuru kwenda haraka na kumkataza kuzungumza na mtu yoyote njiani hata majirani.
Aliongeza baada ya kuondoka kwa muwewe, Amina alikuwa na kawaida ya kwenda kwa waganga wa kienyeji na wakati mwingine waganga hao walifika nyumbani na kila walipofika alimfukuza na kumfungia chumbani hivyo hakujua walikuwa wakifanya nini.
Alitokaje kwenye kifungo
Usiku wa Kuamkia Alhamisi ya Juni 5, binti huyo alifanikiwa kutoka katika ‘kifungo’. Majirani wa Amina ambao walishidwa kuendelea kuvumilia kusikia sauti za kilio cha Yusta mara kwa mara hasa nyakati za usiku.
Majirani hao waliamua kupeleka taarifa za jambo hilo kwa taasisi isiyo ya kiserikali ya Jipange ambayo inafanya shughuli za kutetea wanawake. Baada ya kupata taarifa hizo, Jipange walitoa taarifa polisi na hapo ndipo mtego wa kumnasa Amina uliwekwa na hatimaye majira ya saa 8:00 usiku alikamatwa akiwa katika harakati za kukimbia na kumtorosha Yusta ili kuficha ushahidi.
Mwenyekiti wa Jipange, Janet Mawinza alisema walipopata taarifa za Yusta kutoka kwa wasamaria wema, waliwashirikisha polisi, lakini kwa bahati mbaya taarifa zilivuja na kumfikia mtuhumiwa hivyo alipanga njia ya kutoroka.
“Tulifika nyumbani kwa Amina majira ya usiku ili kulinda mtu asitoke, lakini kumbe yeye alishafahamu ujio wetu, hivyo aliruka dirisha na kukimbia. Alimkabidhi Yusta kwa kijana aliyetayarishwa kumtorosha.”

Anaendelea kusema kwa bahati nzuri kwa kushirikiana na majirani tulifanikiwa kuwazidi nguvu na hivyo mwendesha pikipiki aliyekuwa akimtorosha Amina alikimbia na sisi kufanikiwa kumkamata. Hivyo ilimlazimu na yule kijana aliyeondoka na Yusta kumpeleka kituo cha polisi.”
Polisi wazungumzia
Mkaguzi msaidizi polisi wa Dawati la Jinsia, Mkoa wa Kinondoni, Prisca Komba alisema suala la Yusta limefikishwa polisi kituo cha Oystebay na mshitakiwa tayari amekamatwa na kufunguliwa jalada namba OB/RB/9967/2014 kwa kosa la kujeruhi na upelelezi utakapokamilika litapelekwa mahakamani kwa hatua zaidi. Kauli hiyo imeungwa mkono na kaimu kamada wa polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Thobias Edoyeka.
Alisema taarifa za binti huyo ziliwafikia baada ya majirani kuzipeleka kwa kikundi kinachojulikana kwa jina la Jipange kilichopo maeneo hayo ya Kwamanjunju na kikundi hicho kutoa taarifa polisi na ndipo mtego wa kumnasa mwanake huyo ukawekwa.
Alisema majirani walikuwa wakisikia kelele za kilio mara kwa mara zikitokea ndani ya nyumba ya mtuhumiwa.
“Tumekagua makovu na majeraha mbalimbali yaliyo katika mwili wake na kupata jumla kuwa yako 91,” alisema Prisca.
”Tangu tumempata, amekuwa akinitaka nisiondoke mbali naye kwa kuwa ana hofu. Lakini sasa afadhali kidogo baada ya kumpatia ushauri na kumuhakikishia kwamba hapa yuko salama.”
Afisa wa Ustawi wa Jamii wa Mwananyamala, Rose Temu naye alisema suala la Yusta liko mikononi mwao na wanafuatilia kwa karibu matibabu pamoja na usalama wake.
Akutana na mama yake
Siku ya Jumapili Juni 8 Mwananchi ilimtembelea Yusta kwa mara ya pili. Ilikuwa ni muda wa kuona wagonjwa saa 6:00 mchana kumbe miongoni mwa watu waliohitaji kumuona, alikuwepo na mama yake mzazi aitwaye Modesta Simon.
Ilikuwa ndio mara ya kwanza kwa wawili hao kukutana baada ya miaka mitatu ya mateso. Modesta alifika jijini akitokea Tabora kwa lengo la kumwona binti yake baada ya kusikia taarifa zake kupitia vyombo vya habari na ndugu yake aliyeko Arusha.
Ulikuwa ni wakati wa furaha na huzuni. Ulikuwa wakati mgumu kwa mama huyo kuamini hali aliyomkuta nayo mwanae. Vilio vilitawala hali iliyowafanya ndugu wa baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika wodi hiyo kujaa katika kitanda cha Yusta.

Mara baada ya mama huyo kuingia wodini, Yusta aliyekuwa ameketi kitandani aliruka na kumkimbilia mlangoni na kilichofuata ilikuwa vilio.
Akizungumza huku akimkagua mwilini na kutokwa na machozi, Modesta alisema: “Jamani, Amina kweli amekufanya hivi. Kila nikiuliza wananiambia hujambo kumbe umeharibika hivi?
“Amina ni mtoto wa mjomba wangu kabisa na sikuwahi kuambiwa chochote, niliamini mnaishi vizuri. Sikudhani kama anaweza kulifanya jambo hili.”
Modesta alisema awali alikuwa na mawasiliano na mwanae kwa kutumia simu ya mama yake Amina ambaye wanaishi karibu, lakini hivi karibuni alianza kupata wasiwasi baada ya kila alipohitaji kuongea naye, alipewa sababu hivyo akaomba Yusta kurudishwa na aliahidiwa angepelekewa mwezi huu.
“Alinihahidi mwezi huu angemleta Yusta nyumbani. Alisema anataka amnunulie cherehani ili akija apate shughuli ya kufanya,” alisema.
Alisema anaviachia vyombo vya sheria katika kumpatia haki binti yake na anatamani kuona Amina anaadhibiwa kulingana na kosa alilolitenda.
Kwa upande wake, Yusta alisema amefurahi kukutana na mama yake kwani sasa ataweza kumweleza mateso yake yote kiundani.
“Nimefurahi polisi waliponiambia mama anakuja, sasa nina furaha zaidi nimemuona... nitaweza kuongea naye. Sikuweza kumueleza kwenye simu kwa sababu Amina alikuwa akinisimamia kila aliponipa simu niongee naye,” alisema.
“Madakatari wameniambia nimeruhusiwa. Mama akiondoka nataka twende wote, sitaki tena kubaki hapa”
Yusta alisema akipata pesa za mtaji angependa kujishughulisha na utengenezaji batiki na pia ushonaji, kwani hizo ndizo fani anazozipendelea zaidi katika maisha yake.
Afisa muuguzi katika wodi aliyolazwa Yusta, Erica Massawe alisema hali ya binti huyo imeimarika na tayari alisharuhusiwa kutoka tangu Juni 6, hivyo wanasubiri maelekezo ya polisi na Ustawi wa Jamii ambao ni wahusika wakuu katika shauri la binti huyo.
“Tunasubiri polisi ili tuwapatie hati ya ruhusa (discharge) na PF 3 kwani haturuhusiwi kumkabidhi kwa ndugu, hata akitembelewa anakuwa chini ya uangalizi wetu,” alisema.

Usuli
Yusta alitoka hospitali Jumatatu ya Juni 9 na kukabidhiwa kwa kikundi cha wanahakarati wa kutetea haki za wanawake (Jipange) baada ya majadiliano baina ya mama yake, kamati ya ulinzi na usalama kata ya makumbusho na ofisa mtendaji kata ya makumbusho.hii mi kwa ajili ya kurahisisha binti huyo kufika mahakamani pindi atakapohitajika kufanya hivyo.
 
Chanzo: GAZETI LA MWANANCHI

No comments:

Post a Comment