Gari la jeshi la Magereza lenye namba za usajili MT 0033 leo asubuhi majira ya saa 3:30 limemgonga mwananchi mmoja mkazi wa kitongoji cha Marera katika kijiji cha Rhotia wilayani Karatu mkoani Arusha.
Mtu huyo alitambulika kwa jina la Edward Hhando mwenye ameumia vibaya kuanzia maeneo ya kiunoni mpaka miguuni na kwa mujibu wa daktari aliyempa huduma ya kwanza alisema kuwa Bw. Edward amevunjika miguu yote.
Akielezea tukio hilo, shuhuda mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Anderson amesema kuwa wakati ajali ikitokea Bw. Edward alikuwa akivusha mbuzi katika barabara kuu lakini ghafla gari la magereza lilitokea barabarani na kumgonga.
"Dereva ya basi la magereza akakwepa wale mbuzi sasa yeye ndo akawa kwenye wale ng'ombe sasa kule chini ndo akagongwa na gari"
Inaelezwa kuwa mara baada ya kutokea kwa ajali, dereva wa basi la magereza alipiga simu katika kituo cha polisi cha Karatu na kutoa taarifa na kisha baadae kuripoti katika kituo hicho cha polisi kwa aajili ya taratibu zaidi.Aidha, jeshi la polisi limefanya kazi kubwa ya kuhakikisha majeruhi anafikishwa katika hospitali teule ya wilaya kwa kutoa gari la jeshi ili kumsafirisha majeruhi.
Eneo hilo la Marera ni eneo hatari kwa kuwa ni mteremko mkali wenye kona kali na pia mara nyingi ajali hutokea maeneo hayo.
No comments:
Post a Comment