E FM

E FM
SIKILIZA 93.7 E FM KILA SIKU

Sunday, April 27, 2014

WARIOBA ATUNUKIWA NISHANI ILIYOTUKUKA




Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba juzi usiku alikuwa miongoni mwa viongozi na watu mashuhuri waliotunukiwa nishani na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam.


Katika maelezo ya kutoa nishani ya kumbukumbu ya miaka 50 ya Muungano daraja la kwanza, ilielezwa kuwa Jaji Warioba, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliuenzi na bado anauenzi Muungano huo.

“Katiba kipindi chako, pamoja na nyadhifa nyingine, ulikuwa Waziri Mkuu na Makamu wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani…katika kipindi hicho na hadi sasa umeendelea kuwa mwaminifu, umeutunza, umeulinda na umeuenzi Muungano,” ilisema sehemu ya taarifa ya kutoa nishani.

Mbali na Jaji Warioba, wengine waliopewa nishani katika daraja hilo ni Aboud Jumbe Mwinyi aliyekuwa Rais wa Pili wa Zanzibar, Aman Karume, John Malecela, Cleopa Msuya na Dk Salmin Amour Juma.
Wengine ni Omar Ali Juma na Idrissa Abdul Wakil, ambao sasa ni marehemu.
Walioanza kupata tuzo na nishani hizo ni waasisi wa Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Karume(wote ni marehemu) na walioendeleza ambao ni Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.
Wengine waliopewa tuzo ni pamoja na viongozi wa majeshi ya ulinzi na usalama akiwemo Mkuu wa Jenshi la Wananchi (JWTZ), Jenerali Davis Mwamunyange na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu. Wakuu wa JWTZ wastaafu pia walikumbukwa akiwemo, Jenerali Mirisho Sarakikya, Jenerali David Musuguri.
Pia Mama Maria Nyerere naye alitunukiwa nishani hiyo aliyeipokea nishani hiyo kwa niaba ya muasisi wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Nyerere.



Hivi karibuni, Jaji Warioba amekuwa akishambuliwa na baadhi ya Wajumbe wa Bunge la Maalumu la Katiba, pia baadhi ya wanaCCM kutokana na Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliyoiongoza, kupendekeza muundo wa Muungano wa Serikali tatu.

No comments:

Post a Comment