Ripoti mpya imebaini kuwapo kwa unyanyasaji mkubwa wa watoto wanaoshikiliwa kwenye magereza na mahabusu mbalimbali nchini.
Ripoti hiyo yenye kurasa 94 iliyotolewa na Tume ya
Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyochunguza hali za watoto
magerezani na kwenye vituo vya polisi kwa mwaka 2012 na 2013,
imebainisha kuwa walikamatwa kwa makosa mbalimbali yakiwamo wizi wa
kutumia silaha, dawa za kulevya, mauaji, ubakaji na uzururaji.
Timu ya wachunguzi ya tume hiyo ilitembelea
magereza na vituo vya polisi 102 katika mikoa 12 nchini na walikutana na
watoto 570, kati yao wakiwa ni watoto wachanga 47 waliokuwa na mama
zao gerezani.
Ripoti hiyo inaweka wazi kuwa watoto 452 walikutwa
kwenye magereza ya watu wazima kinyume cha sheria, kati yao wavulana
414 na wasichana 38 na kubainisha kuwapo kwa watoto 1,250 wanaozuiliwa
kwenye magereza ya watu wazima, nchi nzima.
“Wavulana 314 na wasichana 37 walikuwa bado
wanasubiri hukumu, lakini watoto 101 (wavulana 100 na msichana mmoja),
walikuwa wameshahukumiwa,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, jumla ya watoto 65
walikutwa wakishikiliwa kwenye mahabusu nne zilizotembelewa, wakiwamo
wavulana 59 na wasichana sita.
“Katika Shule ya Maadilisho ya Mbeya, walikutwa
watoto 36 wote wakiwa ni wavulana, wakati uwezo wa shule ni kuhifadhi
watoto 340 waliohukumiwa,” inaeleza ripoti hiyo.
Inazidi kueleza kuwa hata watoto wadogo ambao bado
wananyonya, wamekuwa wakijikuta kwenye mateso kutokana na wazazi wao
kushikiliwa kwenye vituo vya polisi kwa zaidi ya saa 24.
“Watoto 47 walikutwa vizuizini wakiwa wameambatana
na mama zao. Watoto 17 walikuwa na umri wa chini ya miezi 12,” inaweka
wazi ripoti hiyo.
Iliongeza kuwa watoto waliohojiwa na timu ya
utafiti waliwatupia polisi lawama kwamba wamekuwa wakiwakamata bila
kuwaambia makosa yao, huku wengi wakilalamika kwa kushushiwa kipigo na
kuteswa na polisi hao.
Ripoti inasema kuwa ingawa ni matakwa ya kisheria
kwamba kila mtu anayekamatwa ajulishwe kosa lake, lakini asilimia 79.6
ya watoto waliohojiwa kwenye vituo vya polisi walisema hawakuambiwa
makosa yao.
Jumla ya watoto 182 kati ya 227 waliohojiwa kwenye
magereza ya watu wazima, sawa na asilimia 80, walisema wamekuwa
wakiishi na wafungwa watu wazima na kwamba wakati wa ukaguzi, walikutwa
wafungwa 16,713 katika katika gereza lililostahili kuwa na wafungwa
11,142.
“Hali mbaya zaidi, wakati watoto wanapochanganywa na watu wazima
mchana na usiku. Katika baadhi ya magereza watoto wenye umri chini ya
miaka 18 hutenganishwa na watu wazima wakati wa usiku,” inasema.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC) Dk Helen Kijo-Bisimba, alisema njia pekee itakayowaweka salama
watoto wanaozuiliwa magerezani ni kuwajengea majengo maalumu, ambako
wataishi kwa amani.
Kijo-Bisimba alisema kwa kuwa mtoto anayenyonya,
anahitaji kuwa na mama yake wakati wote hivyo, Serikali inatakiwa kuwapa
wanawake wanaonyonyesha adhabu itakayowaepusha watoto wao na madhara ya
kuishi gerezani.
Alibainisha kuwa, ripoti hiyo itasaidia kufichua
hali ilivyo ndani ya magereza kwa kuwa wanaharakati wengi hushindwa
kwenda kushuhudia mambo yanayoendelea kutokana na sheria kuwazuia
kufanya hivyo.
“Huwa wanasema hakuna watoto wanaochanganywa na
watu wazima, sasa naona ripoti hiyo itasaidia kuweka wazi,” alisema na
kuongeza kuwa Serikali iongeze bajeti ya ujenzi wa magereza.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi
Chanzo: Gazeti la Mwananchi
No comments:
Post a Comment